Latest News
Posted On: Dec 14, 2019

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA

TAARIFA KWA UMMA

TAARIFA YA MIAKA MINNE YA UTEKELEZAJI WA KAZI ZA UDHIBITI WA UBORA NA USALAMA WA BIDHAA CHINI YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO (NOVEMBA 2015 – NOVEMBA 2019)

1.1 UTANGULIZI

Katika kuadhimisha miaka minne (4) ya mafanikio ya utekelezaji wa kazi chini ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) (zamani Mamlaka ya Chakula na Dawa - TFDA) imefanikiwa kufikia na kuvuka malengo iliyojiwekea katika udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii.

TMDA imeweka mifumo na taratibu za ndani za utoaji huduma bora ili kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya ISO 9001:2015 kwa shughuli za kiudhibiti na ISO/IEC 17025:2005 kwa huduma za maabara. Aidha, huduma za TMDA hutolewa kwa kuzingatia viwango vya Mkataba wa Huduma kwa Wateja wa mwaka 2016.

Katika kutekeleza kazi zake kwa kipindi tajwa, TMDA imefanikiwa kama ifuatavyo;

1.2 UDHIBITI WA UBORA, USALAMA NA UFANISI WA DAWA, VIFAA TIBA NA VITENDANISHI

1.2.1 Tathmini na Usajili wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi

Mfumo wa usajili wa bidhaa umeendelea kuimarika ambapo idadi ya bidhaa zilizosajiliwa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika kipindi cha miaka 2015/16 hadi 2018/19, Mamlaka imesajili jumla ya bidhaa 20,247. Hii imetokana na kuongezeka kwa uelewa wa matakwa ya sheria miongoni mwa wafanyabiashara wa bidhaa zinazodhibitiwa na kukua kwa biashara.

1.2.2 Usajili wa majengo na ukaguzi

Mamlaka husajili maeneo ya biashara za bidhaa kwa lengo la kutambua maeneo ambako bidhaa hizo zinazalishwa, kuhifadhiwa, kusambazwa na kuuzwa. Mfumo huu husaidia kuhakikisha kuwa maeneo husika yanakidhi vigezo ili kutoathiri usalama, ubora na ufanisi wa bidhaa.

Katika kipindi cha miaka minne (4), Mamlaka imeweza kusajili jumla ya maeneo 32,860 ya biashara za bidhaa zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na maghala ya kuhifadhi bidhaa, maeneo ya usambazaji, maduka ya jumla na rejareja ya bidhaa.

Aidha, katika kipindi hicho, TMDA imeendelea kutoa msaada wa kiufundi kwa viwanda vilivyopo na kuhusika katika uanzishwaji wa viwanda vipya 12 ambapo kati ya hivyo, viwanda vya dawa za binadamu ni saba (7), viwanda vya dawa za mifugo vinne (4) na kiwanda kimoja (1) cha vifaa tiba na hivyo kuchangia katika uwekezaji nchini.

Jumla ya maeneo 18,753 yanayojihusisha na biashara ya chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi yalikaguliwa ambayo ni ongezeko la 108% ya maeneo 17,250 yaliyokaguliwa kati ya mwaka 2017/18 hadi 2018/2019. Maeneo yaliyokaguliwa ni pamoja na viwanda vya usindikaji, maghala ya kuhifadhia bidhaa, hospitali, vituo vya afya, magari ya kusafirisha bidhaa, maduka ya jumla na rejareja na machinjio mbalimbali.

Kaguzi hizi zililenga kuhakiki ubora wa majengo, mifumo ya utengenezaji na mazingira ya uzalishaji, usambazaji, uhifadhi na uuzaji na hivyo kuimarisha udhibiti wa ubora na usalama wa bidhaa.

1.2.3 Udhibiti wa uingizaji na usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi

Kwa lengo la kuharakisha utoaji wa mizigo bandarini, Mamlaka imeweka wakaguzi wake ambao hufanya kazi masaa 24 kwa siku zote za juma.

Vilevile, TFDA imeweka mfumo wa kieletroniki wa utoaji vibali vya kuingiza na kutoa nchini bidhaa unaomwezesha mteja kutuma maombi, kufanya malipo popote alipo na hatimaye kupata kibali ndani ya masaa 24.

Kwa kutumia mifumo hii, mwenendo wa utoaji wa vibali vya uingizaji na utoaji wa bidhaa nje ya nchi umeongezeka ambapo katika mwaka 2018/19, jumla ya vibali 26,478 vilitolewa sawa na ongezeko la 203% ukilinganisha na vibali 13,018 mwaka 2015/16.

1.2.4 Kuteketeza bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na usalama

Katika mwaka 2017/18, jumla ya tani 140,705.25 za bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba zisizofaa kwa matumizi ya binadamu zenye thamani ya takribani TZS 22,394,078,744 ziliteketezwa ikilinganishwa na tani 664.68 zilizoteketezwa mwaka 2018/19. Hii inaashiria kupungua kwa bidhaa zisizokidhi viwango katika soko la Tanzania.

1.2.5 Ufuatiliaji wa ubora wa dawa na vifaa tiba na udhibiti wa majaribio ya dawa

TMDA hufuatilia, kuondoa na kuteketeza bidhaa ambazo hazikidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi ili kuepusha zisitumiwe na walaji. Kufuatia mpango wa ufuatiliaji wa ubora wa bidhaa katika soko (Post Marketing Surveillance Programme – PMS), sampuli 1,136 za dawa za binadamu zilifuatiliwa na kuchunguzwa katika kipindi cha miaka minne (4) ambapo asilimia 96 ziliendelea kukidhi vigezo vya ubora. Aidha, kati ya sampuli 144 za dawa za mifugo zilizochunguzwa katika kipindi tajwa, asilimia 90 ziliendelea kukidhi vigezo vya ubora.

Kwa upande wa vifaa tiba na vitendanishi, jumla ya sampuli 405 zilichunguzwa katika soko na baada ya uchunguzi ilibainika kwamba sampuli zote zimekidhi vigezo vya ubora. Matokeo haya ni kiashiria kuwa kiasi kikubwa cha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vilivyopo katika soko la Tanzania Bara zinakidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi.

Mamlaka pia imeidhinisha zaidi ya majaribio ya dawa (clinical trials)189 yanayofanyika kwa binadamu hapa nchini ili kuhakikisha yanazingatia sheria, kanuni, miongozo na vigezo vya Kitaifa na Kimataifa. Mfumo wa udhibiti majaribio ya dawa umewezesha TMDA kufahamu idadi na aina ya majaribio yanayofanyika nchini na kulinda haki na afya za watu wanaoshiriki katika majaribio hayo.

1.2.6 Ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa

Mamlaka imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa na vifaa tiba ili kuweza kutambua, kutathmini na kuzuia madhara yasiyovumilika yasitokee kwa wananchi. Aidha, ili kuimarisha upatikanaji wa taarifa hizo, TMDA imeanzisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ADR reporting tool wa utoaji wa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta na njia ya kutuma ujumbe wa simu.

1.2.7 Uchunguzi wa sampuli katika Maabara ya TMDA

Maabara ina jukumu la kufanya uchunguzi wa sampuli za bidhaa kwa lengo la kujiridhisha na ubora na usalama wake kabla ya kufanya maamuzi ya kiudhibiti ndani ya Mamlaka. TMDA imeimarisha shughuli za maabara kwa kuongeza vifaa vya uchunguzi ikiwa ni pamoja na ufungaji wa maabara ndogo 25 zinazohamishika (minilab kits) katika vituo vya forodha kwa ajili ya uchunguzi wa awali wa bidhaa.
Kwa kipindi cha miaka minne (4) matokeo ya uchunguzi wa sampuli yanaonesha kuwa bidhaa zilizochunguzwa zimekidhi viwango vya ubora na usalama kwa wastani wa 90%.

Maabara ya uchunguzi wa dawa imekidhi vigezo vya kimataifa na kutambuliwa rasmi na Shirika la Afya Duniani (WHO prequalification), maabara ya uchunguzi wa maikobiolojia imepata idhibati kwa kiwango cha kimataifa cha ISO/IEC 17025:2005 mwaka 2012 baada ya kukidhi viwango vya mifumo ya maabara vilivyowekwa. Kwa minajili hii majibu ya uchunguzi yanayotolewa na maabara huaminika na hivyo kutambulika Kitaifa na Kimataifa. Hii inamuhakikishia mwananchi uhakika wa maamuzi ya mamlaka kuhusiana na ubora wa bidhaa.

1.3 UTOAJI ELIMU KWA UMMA NA HUDUMA KWA WATEJA

Katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi juu ya kazi na majukumu ya TMDA, njia mbalimbali za utoaji elimu zimekuwa zikitumika ambapo katika kipindi cha 2015/16 – 2018/19 jumla ya wadau 179,856 walipatiwa elimu kupitia njia ya mihadhara (outreach campaigns) katika Mikoa 23 ya Tanzania Bara. Aidha, programu mbalimbali za elimu kwa umma zimerushwa kupitia Televisheni na Redio za kibiashara na kijamii nchini ambapo ujumbe kuhusu matumizi sahihi ya bidhaa ulitolewa kwa wananchi.

Katika kipindi hiki, TMDA pia ilifanya mapitio ya Mkataba wa awali wa Huduma kwa Wateja kwa kupunguza muda wa kutoa huduma zake (service standards) ili kufikia matarajio ya wateja. Vilevile, Mamlaka imeanzisha namba ya kupiga simu bure kwa wateja (Toll free No. 0800 110084) ili kuboresha mawasiliano.

1.4 MIFUMO YA TEHAMA

Mamlaka imeweka mifumo ya utoaji wa huduma kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo taarifa na takwimu za TMDA zikiwemo za bidhaa na majengo yaliyosajiliwa na zile za wateja zimewekwa katika mfumo maalumu (IMIS). Mfumo wa IMIS kwa kiasi kikubwa umerahisisha utoaji huduma za vibali kwa wateja na kwa sasa vibali vinatolewa ndani ya saa 24 ambapo wateja wanaweza kuleta maombi yao kwa mtandao bila kufika ofisi za TMDA.

Mifumo mingine ambayo imewekwa na Mamlaka katika kuboresha utoaji huduma ni pamoja na mfumo mahususi wa usimamizi wa rasilimali watu (HR-MIS), mfumo wa usimamizi wa rasilimali fedha (EPICOR), mfumo wa kusimamia kesi zinazofunguliwa mahakamani, mfumo wa mahudhurio kazini na mfumo wa usimamizi wa taarifa za uchunguzi wa maabara (LIMS).

1.5 USIMAMIZI WA RASILIMALI

Ili kusogeza huduma za kimaabara karibu na wananchi na kupunguza gharama na usumbufu kwa wateja katika Kanda ya Ziwa, TMDA imejenga Maabara kubwa na ya kisasa jijini Mwanza ili kuhudumia mikoa ya Kanda ya Ziwa. Aidha, TMDA imefunga mashine, mitambo na vifaa vya kisasa vyenye thamani ya takriban Tsh. Bil. 5 katika maabara hiyo.

TMDA pia imesimamia vizuri vyanzo vya makusanyo kwa ajili ya udhibiti ambapo bajeti imeongezeka kutoka Tsh. Bilioni 34.64 mwaka 2015/16 hadi kufikia Tsh. Bilioni 53.31 mwaka 2018/19 sawa na 53.8%. Hii imewezesha utoaji huduma kwa ufanisi na kutoa gawio kwa Serikali kila mwaka hadi kufikia Tsh. Bilioni 29.1.

1.6 USHIRIKIANO WA KITAIFA, KIKANDA NA KIMATAIFA

Mamlaka imeendelea kuboresha ushirikiano na Taasisi nyingine za Serikali kwa lengo la kuimarisha udhibiti na kutoa huduma bora kwa wananchi. Aidha, TMDA inashiriki kwenye mipango ya uwianisho wa taratibu za udhibiti wa dawa na vifaa tiba katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Bara la Afrika (SADC). Kupitia Mipango hii, taasisi za udhibiti za nchi wanachama zimekuwa na mifumo thabiti ya pamoja ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba na hivyo kusaidia upatikanaji wa dawa bora, salama na zenye ufanisi.

1.6.1 TMDA kutambulika kimataifa

Kutokana na kuwa na mifumo thabiti ya udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, mnamo mwezi Desemba 2018, TMDA imetambulika kufikia ngazi ya tatu (Maturity Level 3) ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya ubora wa mfumo wa udhibiti wa dawa. Hatua hii imeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia hatua hii.

Pia, TMDA imekuwa mshindi wa kwanza kwa ubunifu wa mfumo wa utoaji huduma kwa wananchi katika Wiki ya Utumishi wa Umma Barani Afrika 2019, na kutunukiwa Tuzo ya ubunifu wakati wa Mkutano wa Umoja wa Nchi za Afrika jijini Nairobi, Juni 2019.

Kwa hatua hizi, TMDA imeweza kushuhudia kufikiwa kwa Dira yake ya kuwa taasisi ya mfano barani Afrika katika udhibiti wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi na hivyo kuvutia nchi mbalimbali kuja kujifunza mifumo iliyopo na kwenda kuitekeleza nchini kwao. Baadhi ya nchi ambazo zimetuma watendaji wa taasisi zao za udhibiti kuja kujifunza mifumo ya utendaji ya TMDA ni pamoja na Zimbabwe, Rwanda, Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini, Botswana, Malawi, Zambia, Mauritius, Lesotho, Madagascar na Bangladesh.

1.7 HITIMISHO

Katika kipindi cha mwaka 2015/16 - 2018/19, Mamlaka imefanikiwa kufikia na kuvuka malengo iliyojiwekea katika utekelezaji wa mipango kazi yake. Mamlaka katika kipindi cha 2019/20 itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji kwa ufanisi wa malengo mahususi nane (8) yaliyomo katika Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5) yaani 2017/18 – 2021/22, ili pamoja na kufikia na kutimiza matarajio ya wateja, pia kuweza kuendelea kulinda afya ya jamii.

Adam M. Fimbo
Kaimu Mkurugenzi Mkuu
5 Desemba, 2019