Latest News
Posted On: Feb 28, 2024


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA

TAARIFA KWA UMMA

27 Februari, 2024

KUONDOA KATIKA SOKO DAWA DUNI YA MACHO AINA YA “XSONE N” MATOLEO NA. 69E00123 NA 69D02323

  1. TMDA inapenda kuutangazia umma kuwa imepokea taarifa kutoka kwa muingizaji na msambazaji wa dawa ya macho aina ya XSONE N (Dexamethasone Sodium Phospate 0.1% w/v & Neomycin Sulphate 0.35% w/v 5 ml) matoleo Na. 69E00123 na 69D02323 inayotengenezwa na kiwanda cha Abacus Parenteral Drugs Limited (APDL), Kampala, Uganda kuwa matoleo hayo yamebainika kutokidhi vigezo vya ubora. Hivyo ni matoleo duni.
  2. Matoleo tajwa yamethibitika kuwa duni kwa kuwa yameonesha kuwa na vipande vidogo vidogo vya rangi ya kahawia (brown) sehemu ya chini ya kifungashio (chupa) tofauti na muonekano wa dawa hiyo ambao ni kimiminika kisicho na rangi yoyote “sterile aqueous, clear, colorless solution”.
  3. Kutokana na kubainika kwa matoleo hayo mawili (2) ya dawa duni, TMDA inatoa maelekezo yafuatayo:-
    1. Wananchi wanaelekezwa kuangalia kwa makini lebo ili kutambua nambari za matoleo ya dawa tajwa na endapo wataona namba za matoleo hayo wasitumie dawa hizo ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
    2. Wauzaji wa dawa (Jumla na rejareja) wanaelekezwa kuyatambua matoleo hayo na endapo watayabaini wasitishe usambazaji na uuzaji wa dawa hizo na kurejesha matoleo hayo walikonunulia.
    3. Vituo vya kutolea huduma za afya na hospitali (Binafsi na umma) wayabainishe na kuyatenga matoleo hayo na kusimamisha matumizi yake na kisha kuyarejesha kwa wasambazaji wake.
  4. TMDA inaendelea kufuatilia ubora wa matoleo mengine ya dawa hii na hivyo inawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa katika ofisi za TMDA nchini ikiwa watabaini uwepo wa dawa inayodhaniwa kuwa duni au bandia katika soko letu ili kuweza kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na utumiaji wa dawa hizo.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Jengo la PSSSF, Ghorofa ya 10, Barabara ya Makole,
S. L. P 1253, Dodoma au
S. L. P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Nukushi: +255 22 2450793
Simu bila malipo: 0800110084