Latest News
Posted On: Apr 13, 2024


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA

TAARIFA KWA UMMA

13 Aprili, 2024

TAARIFA YA KUONDOLEWA (RECALL) KUTOKA KATIKA SOKO KWA DAWA DUNI YA MAJI AINA YA “BENYLIN PEDIATRICS SYRUP” TOLEO NA. 329304

  1. TMDA inapenda kuutaarifu umma kuwa imeona taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii hususan “whatsapp” kuhusu uamuzi wa Mamlaka za Udhibiti wa Dawa (National Medicines Regulatory Authorities) za nchi kadhaa barani Afrika kuzuia matumizi na kuondoa (recall) katika masoko yao kwa dawa duni ya maji aina ya BENYLIN PEDIATRICS SYRUP” toleo Na. 329304 iliyotengenezwa mwezi Mei, 2021 na kiwanda cha Johnson & Johnson (Pvt), Capetown, Afrika ya Kusini (kama inavyoonekana katika picha hapo chini) na ambayo muda wake wa matumizi unaisha mwezi Aprili, 2024.
  2. Dawa hii ya maji kwa kawaida hutumika kuleta nafuu kwa watoto wenye umri kati ya miaka miwili (2) hadi miaka 12 wanapopata dalili au magonjwa yanayotokana na hali ya mzio (allergic conditions) kama vile kukohoa na mafua yanayosababisha homa.
  3. Kufuatia kuwepo kwa taarifa hiyo, TMDA imeanza mara moja kufanya uchunguzi wa dawa husika pamoja na kufuatilia taarifa hii kupitia mifumo yake ya udhibiti wa dawa zinapoingia, kutunzwa, kusambazwa na kutumika nchini ambapo taarifa itatolewa mara matokeo ya uchunguzi na ufuatiliaji utakapokamilika.

  4. Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kuwa toleo hilo la dawa hiyo liliingizwa nchini Aprili mwaka 2022, na kama ilivyoelezwa hapo juu muda wake wa matumizi unaisha mwezi huu (Aprili 2024). Aidha, Ufuatiliaji kwa mwingizaji wa dawa hiyo nchini umebainisha kuwa hakuna tena dawa hiyo katika ghala lake.
  5. TMDA inaendelea kufuatilia ubora wa matoleo mengine ya dawa hii na hivyo inawaelekeza wananchi kuendelea kutoa taarifa katika ofisi za TMDA nchini ikiwa watabaini uwepo wa toleo hilo (329304) katika soko letu ili kuweza kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na utumiaji wa dawa hizo.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Kitalu Na. 56/1, Block E, Kisasa B Centre, Barabara ya Hombolo,
S. L. P 1253, Dodoma au
S. L. P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Nukushi: +255 22 2450793
Simu bila malipo: 0800110084