Latest News
Posted On: Mar 29, 2023


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA
ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA

TAARIFA KWA UMMA

UWEPO KATIKA SOKO WA DAWA BANDIA AINA YA DIOMYCIN 250MG, DIODOL 500MG, DIOCLOX 250MG, MP-CLOXTM 500MG NA INDOZEN 25MG KATIKA VIFUNGASHIO VYA MAKOPO

 1. TMDA inapenda kuutangazia Umma kwamba kupitia mifumo yake ya ukaguzi na ufuatiliaji wa bidhaa katika soko, mnamo tarehe 20 Machi, 2023 ilibaini uwepo katika soko wa dawa bandia za binadamu aina ya Diomycin 250mg, Diodol 500mg, Dioclox 250mg, MP-CloxTM 500mg na Indozen 25mg zikiwa katika vifungashio vya makopo.
 2. Dawa aina ya Diomycin (Erythromycin 250mg) tablets, Diodol (Paracetamol BP 500mg) tablets na Dioclox (Cloxacillin 250mg) capsules zinaonesha kwenye lebo zake kugushiwa kuwa zinatengenezwa na kiwanda cha Keko Pharmaceutical Industries Limited, Dar es Salaam, Tanzania. Dawa aina ya MP-CloxTM 500 (Ampicillin & Cloxacillin 500mg) capsules na Indozen (Indomethacin BP 25mg) capsules zinaonesha kwenye lebo zake kugushiwa kuwa zinatengenezwa na kiwanda cha Zenufa Laboratories Limited, Dar es Salaam, Tanzania.
 3. Ufuatiliaji wa haraka uliofanywa na TMDA katika viwanda tajwa, umebaini kuwa viwanda hivyo havijawahi kutengeneza dawa hizo katika vifungashio vya makopo tangu mwaka 2020.
 4. Dawa bandia hizo ni kama zinavyoonekana kwenye Picha Na. 1, 2, 3 na 4 hapo chini;

  Picha Na. 1: Muonekano wa dawa bandia aina ya Diomycin na Diodol.

  Picha Na. 2: Muonekano wa dawa bandia aina ya Dioclox 250

  Picha Na. 3: Muonekano wa dawa bandia aina ya MP-CloxTM 500

  Picha Na. 4: Muonekano wa dawa bandia aina ya Indozen 25mg

 5. Kutokana na kubainika kwa dawa hizo bandia aina tano (5) wananchi wote wanaelekezwa kuacha kutumia dawa zenye majina hayo ambazo zinachotwa kutoka kwenye makopo na kufungashwa katika mifuko au bahasha za kuwekea dawa, badala yake watumie dawa zilizofungashwa katika blisters (tembe).
 6. Matumizi ya makopo katika kufungasha dawa yalishapigwa marufuku nchini hivyo, wananchi wameaswa kuacha kununua dawa ambazo hazijafungashwa katika blister.
 7. Aidha, TMDA inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha uwepo wa dawa hizo katika soko ambapo hadi sasa watu kadhaa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali kuhusiana na suala hili.
 8. TMDA inaendelea kuwaomba wananchi wote kuendelea kutoa taarifa ikiwa watabaini kampuni, kikundi, mitandao au mtu yeyote anayejihusisha na utengenezaji, usambazaji au uuzaji wa dawa za binadamu katika kifungashio cha kopo.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Jengo la PSSSF, Ghorofa ya 10, Barabara ya Makole,
S. L. P 1253, Dodoma au
S. L. P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Nukushi: +255 22 2450793
Simu bila malipo: 0800110084