Latest News
Posted On: Jul 26, 2021


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




IMETHIBITISHWA KWA: ISO 9001: 2015

TAARIFA KWA UMMA

26 Julai, 2021

UVUTAJI WA TUMBAKU KWENYE MAENEO YANAYOTUMIWA NA WATU WENGI

  1. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekasimishwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto jukumu la kudhibiti bidhaa za tumbaku kuanzia tarehe 30 Aprili, 2021 kupitia Tangazo la Serikali Na. 360.
  2. Kifungu cha 12 cha Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, Sura 121 kimetafsiri maeneo ya umma kama mahali ambapo inatolewa huduma ya afya, maktaba, mahali pa ibada, majengo au maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mikutano ya kitamaduni na kijamii, shughuli za michezo au burudani, sehemu za huduma ya chakula, majengo ya ofisi, vyombo vya usafiri wa anga, ardhi au maji, mabanda ya maonesho, masoko, maduka makubwa na maeneo mengine yoyote yanayotumiwa na umma.
  3. Katika maeneo tajwa, Sheria imekataza uvutaji wa aina yoyote ile wa bidhaa za tumbaku na kuelekeza bango lenye maneno yanayosomeka “NO SMOKING” na “HAIRUHUSIWI KUVUTA SIGARA” kuwekwa.
  4. Hata hivyo, kifungu cha 13 cha Sheria tajwa kimeruhusu uvutaji kwenye baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na taasisi za elimu ya juu, majengo ya ofisi, hoteli, baa, migahawa na maeneo ya burudani ambayo yanapaswa kutenganisha vyumba au maeneo maalum ya kuvutia na kutovutia tumbaku.
  5. Aidha, Kanuni ndogo ya 7 (1) na (2) ya Kanuni za Bidhaa za Tumbaku za mwaka 2014, inawataka wamiliki wote wa majengo yanayotumiwa na watu wengi kuweka vifaa vya kubaini moshi wa tumbaku na kuweka alama zinazosomeka “THIS BUILDING IS INSTALLED WITH A SMOKE DETECTOR” na “JENGO HILI LIMEFUNGWA MITAMBO YA KUBAINI MOSHI WA TUMBAKU”.
  6. Kwa tangazo hili, TMDA inawataka wamiliki, wapangaji na waendeshaji wote wa majengo yanayotumiwa na watu wengi kuhakikisha wanazingatia masharti ya Sheria na Kanuni kama yalivyoainishwa hapo juu.
  7. TMDA inatoa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe ya tangazo hili kwa wamiliki, wapangaji na waendeshaji wa maeneo husika kutimiza masharti ya Sheria na Kanuni kama ilivyoainishwa na baada ya muda huo, ukaguzi utafanyika nchi nzima ili kuhakiki utekelezaji wa maelekezo haya ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria.
  8. Izingatiwe kwamba, bidhaa za tumbaku zinazohusika na tangazo hili ni zile zinazotambulika kisheria ambazo ni sigara, siga, sigarusi, misokoto, kiko na tumbaku ya unga. Bidhaa za tumbaku zisizovutwa (smokeless tobacco products) haziruhusiwi kutumika katika maeneo na mazingira yoyote nchini Tanzania.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
S.L.P 77150, Dar es Salaam au
S.L.P 1253 Dodoma
Simu: +255 222 450512/450751/452108
Simu ya Bure: 0800110084
Nukushi: +255 222 450793
Barua Pepe: info@tmda.go.tz Tovuti: www.tmda.go.tz