Latest News
Posted On: Dec 20, 2019

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA

TAARIFA KWA UMMA

Disemba 20, 2019

UFAFANUZI KUHUSU MIPIRA YA KIUME AINA YA LIFE GUARD ILIYOONDOLEWA KWENYE SOKO NCHINI UGANDA

  1. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inapenda kutoa ufafanuzi kuwa ilipata taarifa kutoka nchini Uganda kuhusu kuondolewa katika soko kwa matoleo mawili ya mipira ya kiume (condoms) aina ya Life Guard (toleo namba 19040205 na 19050105) zilizotengenezwa na kampuni ya MHL Healthcare Ltd ya nchini India na kuingizwa na kusambazwa nchini humo na shirika la Marie Stopes. Matoleo hayo yalikuwa ni sawa na jumla ya paketi 335,000 za mipira ya kiume ambayo uchunguzi wa maabara ulionesha kuwepo na kasoro kwenye ubora kwa kuwa yalikuwa hayakidhi viwango vya ubora.
  2. TMDA inapenda kuutaarifu umma kuwa mipira ya kiume ya Life Guard haijawahi kusajiliwa wala kupewa kibali cha kuingizwa nchini.
  3. Kwa kuzingatia kuwa nchi yetu imepakana na nchi ya Uganda ambapo mipira hiyo ilikuwa inaruhusiwa kuuzwa na kwa kuzingatia uwezekano wa kuingizwa kwa mipira hiyo kupitia njia na mipaka isiyo rasmi maarufu kama ‘njia za panya’, Mamlaka imefanya ukaguzi maalum katika soko nchi nzima katika kipindi cha mwezi Novemba – Disemba, 2019.
  4. Katika ukaguzi huo tumekamata jumla ya paketi za mipira ya kiume ya Life Guard 6756 zilizokuwa zimeingizwa nchini kwa njia zisizo rasmi katika maeneo 782 yaliyokaguliwa nchi nzima. Mipira hiyo imekamatwa katika mikoa ya Njombe (paketi 240), Singida (paketi 24), Mwanza (paketi 696), kituo cha Forodha cha Mutukula mkoani Kagera (paketi 5796). Wamiliki wa maduka yaliyokutwa yanauza mipira hiyo wamefikishwa kwenye vyombo vya usalama kwa mujibu wa sheria na tayari majalada ya kesi dhidi ya wamiliki wa maduka hayo yamefunguliwa.
  5. Ukaguzi katika maeneo yote ya biashara unaendelea nchi nzima ili kubaini uwepo wa mipira ya kiume aina ya Life Guard na kuiondoa katika soko. Pia usimamizi wa mipaka unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuzuia uingizaji wa mipira hiyo ya kiume pamoja na bidhaa nyingine zisizoruhusiwa kutumika nchini. Aidha hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa wafanyabiashara wote watakaokutwa wanamiliki au kuuza bidhaa hizo kwenye maeneo yao ya biashara.
  6. Wananchi mnaombwa kutoa taarifa endapo mtaona mtu anauza mipira ya kiume aina ya Life Guard ili hatua ziweze kuchukuliwa haraka kwa lengo la kulinda afya ya jamii.
  7. Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana nasi kupitia Ofisi za Makao Makuu au Ofisi za Kanda zilizoko Dodoma, Mwanza, Tabora, Simiyu, Mbeya, Arusha, Mtwara na Dar es Salaam.
Imetolewa na:
Kaimu Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Mtaa wa Mwanza, Kitalu T, Kiwanja Na.6
S.L.P 1253, Dodoma Au
S.L.P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Simu bila Malipo: 0800110084