Latest News
Posted On: Jan 05, 2022
|
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA |
|
IMETHIBITISHWA KWA: ISO 9001: 2015
TAARIFA KWA UMMA
5 Januari, 2022
TAHADHARI YA UWEPO WA MATAPELI KWA WATEJA WA TMDA
- Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inapenda kuutadharisha umma kuwa wamejitokeza matapeli ambao hujifanya kuwa ni watumishi wa TMDA. Watu hao hupiga simu au kutuma ujumbe mbali mbali kwa mfano “Habari – TMDA tunapenda kukujulisha huduma ipo tayari wasiliana nasi kwa namba hii ahsante”;
- Matapeli hao hudai kuwa wanaweza kuwasaidia wateja kupata huduma zinazotolewa na TMDA kwa muda mfupi kuliko muda ulioainishwa katika Mkataba wa Huduma kwa Mteja. Baada ya kutoa taarifa hiyo, hutuma ujumbe mwingine au kupiga simu na kuomba kiasi fulani cha fedha ikiambatana na namba ya simu ambayo pesa hizo zinapaswa kutumwa;
- TMDA inachukua fursa hii kuutahadharisha umma juu ya utapeli huo na kushauri kupuuza ujumbe wowote wa aina hiyo. Aidha, tunawakumbusha wateja kuwa huduma zetu hutolewa katika ofisi ya Makao Makuu Dodoma, ofisi ndogo ya Makao makuu Dar es Salaam, ofisi za kanda zilizopo Dar Es Salaam, Arusha, Dodoma, Geita, Mbeya, Mwanza, Mtwara na Tabora pamoja na vituo vya forodha na siyo kwa kificho kama ambavyo matapeli wanataka ieleweke;
- Vile vile, huduma hizo hutolewa na mtumishi anayevaa kitambulisho na beji yenye jina la mtumishi husika ili iwe rahisi kwa mteja kumtambua pale inapohitajika;
- Kwa tangazo hili, umma unakumbushwa kuendelea kupata huduma katika ofisi zetu zilizoko nchini kote na kuhakikisha kuwa malipo yote ya ada na tozo yanafanyika kupitia benki au mawakala waliothibitishwa na benki husika baada ya kupatiwa ankara kifani (Profoma invoice) na Namba ya Malipo ya Serikali (Control Number);
- Aidha, tunawashauri wateja kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya matapeli hao na pale wanaposhawishiwa kupatiwa huduma nje ya ofisi za TMDA na kwa utaratibu tofauti, wasisite kutoa taarifa mara moja katika ofisi za TMDA nchini kote, kupiga simu bila malipo kupitia Na. 0800110084 au kutoa taarifa kituo chochote cha Polisi kilicho karibu; na
- TMDA inashirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama kuwatafuta matapeli hao ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
S.L.P 77150, Dar es Salaam au
S.L.P 1253 Dodoma
Simu: +255 222 450512/450751/452108
Simu ya Bure: 0800110084
Nukushi: +255 222 450793
Barua Pepe: info@tmda.go.tz Tovuti: www.tmda.go.tz