Latest News
Posted On: Oct 07, 2022


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




IMETHIBITISHWA KWA: ISO 9001: 2015

TAARIFA KWA UMMA

07 Oktoba, 2022 Dodoma

Tahadhari ya Dawa Zenye Madhara na Kusababisha Vifo

  1. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu uwepo wa dawa tajwa hapa chini ambazo zimeonekana kuwa na viambata vinavyosababisha madhara ya kiafya ikiwa ni pamoja na vifo kwa watumiaji (hasa watoto).
  2. Dawa husika ni hizi zifuatazo - Promethazine Oral Solution, Kofexmalin Baby Cough Syrup, Makoff Baby Cough Syrup na Magrip N Cold Syrup.
  3. Dawa zote hizi zinazotengenezwa na kiwanda chenye jina Maiden Pharmaceuticals Limited kilichoko nchini India zimepimwa na kukutwa na viambata vijulikanavyo kama diethylene glycol na ethylene glycol. Viambata hivi husababisha madhara na hata vifo kwa watumiaji.
  4. Dawa hizi zimeonekana kwenye soko la nchini Gambia na kwa mujibu wa WHO inasadikika watoto takribani 66 wa nchi hiyo wamefariki kutokana na matumizi ya dawa hizi.

  5. TMDA inapenda kuuhakikishia umma wa watanzania kwamba dawa hizi zote haziko kwenye soko la nchi yetu na hazijawahi kusajiliwa ili kutumika hapa nchini.
  6. Hata hivyo, Mamlaka inaendelea kuchukua tahadhari zote kupitia mifumo yake ya udhibiti ili kubaini endapo dawa hizi zitafika nchini kwetu.
  7. Wito unatolewa kwa wananchi kutoa taarifa kwenye Ofisi za TMDA zilizoko karibu, Ofisi za Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya au Vituo vya Polisi endapo yeyote atabaini kuziona mahali popote ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa. Muonekano wa makasha ya nje ya dawa husika umeainishwa hapa chini.
  8. Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kupitia Ofisi za TMDA Makao Makuu au Ofisi za Kanda zilizoko Mwanza, Geita, Arusha, Mbeya, Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara na Tabora na unaweza pia kupiga simu bila malipo kupitia Na.0800110084.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Kiwanja Na. 56/1, Barabara ya Swaswa,
Mkabala na Shule ya Martin Luther,
S.L.P 1253, Dodoma.
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Simu bila Malipo: 0800110084
Barua pepe: info@tmda.go.tz
Tovuti: www.tmda.go.tz