Latest News
Posted On: May 14, 2024


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA
ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA

TAARIFA KWA UMMA

9 Mei, 2024

MATOKEO YA UFUATILIAJI WA UBORA NA USALAMA WA DAWA YA MAJI AINA YA “BENYLIN PEDIATRIC SYRUP” TOLEO NA. 329304

  1. Mnamo tarehe 13 Aprili, 2024, TMDA ilitoa tangazo kwa umma juu ya ubora na usalama wa dawa ya maji aina ya ‘’BENYLIN PEDIATRIC SYRUP” toleo Na. 329304 inayotengenezwa na kiwanda cha Johnson & Johnson (Pvt), Capetown, South Afrika. Dawa hii hutumika kuleta nafuu kwa watoto wenye umri kati ya miaka miwili (2) hadi miaka 12 wanapopata dalili au magonjwa yanayotokana na hali ya mzio (allergic conditions) kama vile kukohoa na mafua yanayosababisha homa.
  2. Toleo hilo lilitengenezwa mwezi Mei, 2021 na tarehe ya mwisho wa matumizi yake ilikuwa mwezi Aprili, 2024. Ilidaiwa kuwa baada ya uchunguzi wa kimaabara, dawa hiyo ilibainika kuwa na kiasi kisichokubalika cha viambata (vichafuzi) aina ya Diethylene Glycol na Ethylene Glycol vinavyoweza kusababisha madhara ya kiafya ikiwa ni pamoja na vifo kwa watumiaji.
  3. Kufuatia kuwepo kwa taarifa hiyo, TMDA iliahidi kufanya uchunguzi wa kina wa dawa husika na inapenda kuwajulisha kuwa toleo tajwa (329304) pamoja na matoleo mengine ya dawa ya ‘’BENYLIN PEDIATRIC SYRUP” hayana tatizo lolote la ubora, usalama na ufanisi.
  4. Kwa matokeo haya, wananchi waendelee kuitumia kama kawaida. Aidha, wauzaji wa dawa (jumla na rejareja) wanaelekezwa kuendelea kusambaza na kuuza matoleo ya dawa tajwa yaliyopo kwenye soko. Vile vile, vituo vya kutolea huduma za afya na hospitali (binafsi na umma) viendelee na matumizi ya dawa tajwa.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Kitalu Na. 56/1, Block E, Kisasa B Centre, Barabara ya Hombolo,
S. L. P 1253, Dodoma au
S. L. P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Nukushi: +255 22 2450793
Simu bila malipo: 0800110084