Latest News
Posted On: May 24, 2022


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




IMETHIBITISHWA KWA: ISO 9001: 2015

TANGAZO KWA UMMA

20 Mei, 2022

KATAZO LA MATANGAZO YA BIASHARA YANAYOHUSU BIDHAA ZA TUMBAKU

  1. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Wakala wa Serikali iliyopewa jukumu la kudhibiti bidhaa za tumbaku kupitia Tangazo la Serikali Na. 360 tangu tarehe 30 Aprili 2021, inapenda kuwajulisha wateja na wadau wetu kuwa imebaini uwepo wa matangazo ya bidhaa ya tumbaku ijulikanayo kama “Tembo Cigarette’’ kupitia magazeti na akaunti binafsi ya Instagram ya msanii mmoja wa muziki wa kizazi kipya.
  2. Matangazo hayo ni kinyume na kifungu cha 17(3) cha Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121. Kifungu hicho kinakataza mtu au taasisi yoyote kutangaza bidhaa za tumbaku isipokuwa kwa maudhui ambayo yanalenga kuelimisha umma juu ya athari za kiafya zitokanazo na matumizi ya bidhaa hizo.
  3. Mamlaka inapenda kuchukua fursa hii kuukumbusha umma kuacha mara moja kufanya shughuli zozote zenye lengo la kutangaza au kuhamasisha matumizi ya bidhaa za tumbaku nchini kwa kuwa bidhaa hizi zina madhara kiafya.
  4. Aidha, Mamlaka inawataka wamiliki wa vyombo vya habari nchini na wasanii kuacha mara moja kurusha matangazo yoyote yanayohusu bidhaa za tumbaku isipokuwa yale yenye kibali na TMDA.
  5. Natarajia ushirikiano katika suala hili.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba
S.L.P. 1253 Dodoma au 77150 Dar es salaam
Simu: +255 22 2450512/2450751/2452108
Nukushi: +255 22 2450793
Barua pepe: info@tmda.go.tz; Tovuti: www.tmda.go.tz