Latest News
Posted On: Sep 14, 2026
|
TJAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA |
|
ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA
TAARIFA KWA UMMA
14 Septemba, 2026
UWEPO KATIKA SOKO WA CHANJO BANDIA YA MIFUGO AINA YA “TEMEVAC NDV STRAIN 1-2”
- Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inapenda kuutangazia umma kuwa, kwa kushirikiana na Tanzania Veterinary Laboratory Agency (TVLA), imefanikiwa kubaini uwepo wa chanjo bandia aina ya Temevac NDV Strain 1-2.
- Uchunguzi umebainisha kuwa chanjo hiyo bandia haikuzalishwa na TVLA na inasambazwa na wafanyabiashara wasiowaaminifu wakitumia lebo zilizogushiwa za chanjo halisi ya Temevac NDV Strain I-2.
- Aidha, chanjo hiyo bandia ina mapungufu mbalimbali kama ifuatavyo: -
- Kwenye chanjo halisi, nembo ya TVLA ina picha ya darubini (microscope), wakati chanjo bandia ina picha ya kuku;
- Upande wa kushoto wa lebo ya chanjo halisi una mng’ao wa aluminiamu, wakati chanjo bandia haina; na
- Lebo ya chanjo halisi ina taarifa zote muhimu ikijumuisha tarehe ya kutengenezwa, tarehe ya kuisha muda wa matumizi, na namba ya toleo, wakati chanjo bandia haina namba ya toleo.
- Muonekano wa chanjo hiyo bandia ukilinganishwa na halisi umeonyeshwa kwenye picha hapa chini.
- Wauzaji wote wa dawa za mifugo (wa jumla na rejareja) pamoja na wamiliki wa kliniki za mifugo wanashauriwa kukagua lebo za chanjo hizo kwa umakini mkubwa. Endapo chanjo hiyo itabainika, inaelekezwa kusitisha matumizi yake mara moja ili kuepusha madhara kwa mifugo, na kutoa taarifa haraka katika ofisi za TMDA zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Songea, Tabora, na Geita, au kupitia barua pepe: info@tmda.go.tz, au simu ya bila malipo (0800110084).
- Aidha, TMDA inatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu au makampuni yanayojihusisha na usambazaji wa bidhaa tiba bandia, duni, zisizosajiliwa, au zisizofaa kwa matumizi ikiwemo zile zilizokwisha muda wake wa matumizi (expired).
- TMDA itaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kulinda afya ya jamii na mifugo kwa kuhakikisha kuwa dawa zote zinazopatikana nchini zinakidhi viwango vya ubora, usalama, na ufanisi unaotakiwa.
Chanjo Bandia
Maelezo katika lebo yameandikwa kwa lugha ya Kiingereza
Chanjo Halisi
Maelezo katika lebo yameandikwa kwa lugha ya Kiswahili
Jina la bidhaa bandia mwishoni ni 1-2
Jina la bidhaa halisi mwishoni ni I-2
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Kitalu Na. 56/1, Block E, Kisasa B Centre, Barabara ya Hombolo,
S. L. P 1253, Dodoma au
S. L. P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Nukushi: +255 22 2450793
Simu bila malipo: 0800110084