Latest News
Posted On: May 31, 2026


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA

TANGAZO KWA WAINGIZAJI BIDHAA NCHINI

28 Mei, 2026

UFAFANUZI WA CHANGAMOTO ZA MFUMO MPYA WA PAMOJA WA UGOMBOAJI WA MIZIGO (TANESW)

  1. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ilianza kutumia mfumo mpya wa ugomboaji wa mizigo wa pamoja ujulikanao kama Tanzania Electronic Single Window (TANESW) mnamo tarehe 1 Mei, 2026.
  2. Lengo kuu la hatua hii ni kurahisisha ugomboaji wa shehena za mizigo mbalimbali inayoingizwa nchini zikiwemo bidhaa tiba. Aidha, utaratibu huu unalenga kuhakikisha kuwa ugomboaji wa shehena hizo unafanyika kwa kutumia mfumo mmoja badala ya kuwa na mifumo mingi, suala ambalo lilikuwa ni usumbufu kwa wateja.
  3. Baada ya kuanza kutumika kwa mfumo huu, kumejitokeza changamoto mbalimbali za kimfumo kama ifuatavyo; -
    1. Wateja kuwa na uelewa mdogo wa namna ambavyo mfumo mpya unavyofanya kazi;
    2. Kucheleweshwa kwa ugomboaji wa mizigo ambayo ina bidhaa zisizodhibitiwa na TMDA;
    3. Kucheleweshwa kwa ugomboaji wa mizigo iliyochanganywa na bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA;
    4. Kucheleweshwa kwa ugomboaji wa mizigo ambayo tayari ilikuwa na vibali vya kuingiza mizigo vilivyotolewa na TMDA kabla ya mfumo mpya kuanza kutumika; na
    5. Kutoonekana kwa hoja ambazo zimetumwa kwa wateja kupitia mfumo wa TANESW na hivyo mteja kushindwa kujibu hoja hizo kwa wakati.
  4. Ili kutatua changamoto hizo, katika kipindi hiki cha mpito, TMDA inafanya yafuatayo: -
    1. Kuruhusu mizigo yote ambayo haidhibitiwi na TMDA igombolewe kupitia mfumo wa TANOGA;
    2. Kuruhusu mizigo yote yenye vibali vilivyotolewa kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo huu mpya, kuingizwa nchini bila kulazimika kutumia mfumo mpya wa TANESW;
    3. Kushirikiana na TRA kutatua changamoto ya kutoonekana kwa hoja zinazotumwa kwa baadhi ya wateja; na
    4. Kuweka dawati la msaada kwa wateja (help desk) katika vituo vya forodha vya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na ofisi za bandari zilizopo TPA Tower - ghorofa ya 3, ili kusaidia kutatua changamoto za kimfumo.
  5. Wito unatolewa kwa wateja wetu kuwasiliana na TMDA pale wanapokumbana na changamoto za matumizi ya mfumo huu mpya kupitia namba 0784 227 069 (Meneja, Udhibiti na Ukaguzi wa Vifaa Tiba), 0782 119 437 (Meneja, Udhibiti na Ukaguzi wa Dawa) na 0784 040 655 (Meneja, TMDA, Kanda ya Mashariki).
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
S.L.P 1253, Dodoma
Simu+255 (26) 2961989/2061990
Barua pepe: info@tmda.go.tz
Tovuti: www.tmda.go.tz
Simu bila malipo: 0800110084