Latest News
Posted On: Jul 28, 2024


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA

TAARIFA KWA UMMA

27 Julai, 2024

UFAFANUZI KUHUSU UVUMI JUU YA DAWA YA PARACETAMOL INAYODAIWA KUBABUA NGOZI

  1. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa tiba nchini.
  2. Ili kuhakikisha kuwa bidhaa tiba (zikiwemo dawa) zilizoko katika soko nchini zinakidhi matakwa ya usalama, ubora na ufanisi, TMDA imeweka mifumo mbalimbali ya udhibiti ikiwa ni pamoja na tathmini na usajili, ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara na ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa katika soko.
  3. Mamlaka imebaini uwepo wa taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa dawa aina ya paracetamol ambayo imeandikwa P 500 na kudaiwa kubabua ngozi kama inavyooneshwa katika picha hapo juu. Dawa hiyo inadaiwa kuwa ni ‘’paracetamol mpya nyeupe sana na inayong'aa, madaktari wanashauri kuwa ina virusi vya "Machupo", inayochukuliwa kuwa moja ya virusi hatari zaidi ulimwenguni, na kiwango cha juu cha vifo.
  4. Mtoa taarifa anaitaka jamii kuisambaza taarifa hii kwa kila mtu aliyeko katika orodha yake ya mawasiliano ili kuokoa maisha. Anamalizia kwa kusema ‘’Nimefanya sehemu yangu, sasa ni zamu yako. Kumbuka kwamba Mungu huwasaidia wale wanaosaidia wengine. ‘’Sambaza kama ilivyopokelewa’’.
  5. Taarifa hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara na TMDA imekuwa ikitolea ufafanuzi ikiwemo taarifa ya mnamo tarehe 10 Mei, 2023 juu ya dawa aina ya P-500® (PARACETAMOL) ya Apex Laboratories Private Limited, Tamil Nadu, India iliyodaiwa kuwa na virusi hivyo.
  6. TMDA inapenda kuufahamisha Umma kwa mara nyingine kwamba hakuna virusi vinavyojulikana kwa jina la Machupo. Aidha, virusi vya aina yoyote haviwezi kuishi kwenye kidonge.
  7. Dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu zilizopo katika soko nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara zimesajiliwa baada ya kuthibitishwa kuwa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi unaotakiwa na hivyo, ni salama kwa matumizi yaliyoainishwa.
  8. TMDA inapenda kuwahakishia wananchi kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda afya ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa bidhaa tiba zinazotumika nchini ni zile zenye kukidhi matakwa ya ubora, usalama na ufanisi.
  9. Vilevile, Mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kupata ufafanuzi kutoka kwenye mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zinazoweza kuleta taharuki kwenye Jamii.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Kitalu Na. 56/1, Block E, Kisasa B Centre, Barabara ya Hombolo,
S. L. P 1253, Dodoma au
S. L. P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Nukushi: +255 22 2450793
Simu bila malipo: 0800110084