Latest News
Posted On: Aug 20, 2026
|
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA |
|
ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA
TAARIFA KWA UMMA
20 Agosti, 2026
TAARIFA KUHUSU DAWA ZOTE ZENYE KIAMBATA HAI CHA KETAMINE KUWEKWA KWENYE KUNDI LA DAWA TIBA ZENYE ASILI YA KULEVYA
- Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inapenda kuwataarifu wateja na wadau wake wote kwamba Mhe. Waziri wa Afya ameidhinisha Kanuni za Makundi ya Dawa za mwaka 2026, TS. Na. 150 tarehe 19 Juni 2026.
- Kanuni zilizoidhinishwa zinabadili Kanuni zilizokuwa zikitumika hapo awali za mwaka 2015, TS. Na. 63
- Kanuni hizi mpya zimefanya mabadiliko ya kundi la dawa zenye kiambata hai kijulikanacho kama Ketamine kutoka dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari (POM) kwenda kundi la dawa zenye asili ya kulevya (narcotic drug).
- Kwa mabadiliko haya, kuanzia tarehe ya tangazo hili, dawa zote zenye kiambata husika zitaanza kudhibitiwa kama dawa zenye asili ya kulevya.
- Kwa mantiki tajwa, wale wote wanaohusika na kutengeneza, kuagiza, kusambaza na kuuza dawa husika watapaswa kufuata taratibu zote kama ambavyo zinahusika kwa dawa zenye asili ya kulevya.
- Taratibu hizo ni pamoja na dawa husika zitakuwa zikiingizwa nchini na Bohari ya Dawa (MSD) pekee na kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoidhinishwa na TMDA.
- Kwa tangazo hili na kama sehemu ya kujipanga kusimamia vizuri suala hili, wale wote wenye dawa husika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kama famasi za jumla na rejareja, wanaelekezwa kuwasilisha TMDA idadi ya dawa walizonazo ili kuweza kufahamu kiwango halisi kilichopo nchini hadi sasa. Taarifa husika ziwasilishwe hadi kufikia tarehe 1 Septemba 2026.
- Baada ya kupokea taarifa za idadi iliyopo, TMDA itatoa maelekezo katika siku za karibuni ya kusitisha kabisa matumizi ya dawa zenye Ketamine kwenye maduka binafsi ya jumla na rejareja na yasiyoruhusiwa kuhifadhi na kuuza dawa husika.
Director General,
Tanzania Medicines and Medical Devices Authority
P.O. Box 1253, Dodoma.
Tel; +255 222 450512/658 445222/777 700002
Fax: +255 222450793
Email: info@tmda.go.tz
Website: www.tmda.go.tz