Latest News
Posted On: Feb 08, 2022


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




IMETHIBITISHWA KWA: ISO 9001: 2015

TAARIFA KWA UMMA

08 Februari, 2022

UFAFANUZI KUHUSU USALAMA WA DAWA ZINAZOTUMIKA KATIKA VITUO VYA AFYA NA ZAHANATI NCHINI

  1. Hivi karibuni kumekuwa na taarifa zinazosambaa kupitia mitandao ya kijamii pamoja na vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na usalama na ubora wa dawa zinazotumika katika zahanati na vituo vya afya hapa nchini.
  2. Chimbuko la taarifa hiyo limetokana na ripoti ya ukaguzi kwa baadhi ya majengo ya kuuzia dawa katika Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha mwezi Juni – Desemba 2021 iliyowasilishwa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya (RCC) kilichofanyika tarehe 17 Januari 2022. Ripoti iliyowasilishwa ililenga kuwafikia watendaji ambao hufanya kazi moja kwa moja na TMDA ambapo lengo la kuwashirikisha lilikuwa ni kujadiliana namna bora ya kuimarisha ukaguzi wa vituo vya afya na zahanati ili kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
  3. TMDA inapenda kutoa ufafanuzi kuwa taarifa juu ya 80% ya usalama wa dawa ilipotoshwa. Taarifa halisi ilihusu maeneo mahususi pekee yaliyokaguliwa na ofisi ya TMDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo yalihusisha hospitali 13, vituo vya afya 8, zahanati 29, maduka ya dawa 167 na Maabara 34 katika mkoa wa Mbeya kwa kipindi tajwa na si uwakilishi wa nchi nzima kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa na vyombo vya habari.
  4. Mamlaka inawahakikishia umma kwamba inayo mifumo thabiti ya ufuatiliaji wa usalama, ubora na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vilivyopo katika soko ambapo katika kipindi cha mwaka 2020/21 takwimu za nchi nzima zinaonesha kuwa 89% ya bidhaa za dawa na 99% kwa vifaa tiba na vitendanishi zilizopo katika soko ikiwa ni pamoja na zahanati na vituo vya afya zinakidhi vigezo.
  5. TMDA inatoa wito kwa vyombo vya habari kupata ufafanuzi wa Mamlaka kuhusiana na taarifa zinazohusu dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa za tumbaku ili kujiridhisha na usahihi wa taarifa na kuepuka upotoshaji na taharuki kwa jamii.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
S.L.P 77150, Dar es Salaam au
S.L.P 1253 Dodoma
Simu: +255 222 450512/450751/452108
Simu ya Bure: 0800110084
Nukushi: +255 222 450793
Barua Pepe: info@tmda.go.tz Tovuti: www.tmda.go.tz