Latest News
Posted On: Jan 13, 2024


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA




ISO 9001: 2015 IMETHIBITISHWA

TAARIFA KWA UMMA

12 Januari, 2024

UFAFANUZI KUHUSU DAWA DUNI YA VIDONGE AINA YA FLUCONAZOLE MILIGRAMU 200 INAYOZALISHWA NA KIWANDA CHA UNIVERSAL CORPORATION CHA KIKUYU, KENYA KATIKA SOKO LA TANZANIA

  1. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya iliyoanzishwa chini ya Kifungu cha 4 (1) cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura, 219. TMDA inajukumu la kulinda afya ya Jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, na vitendanishi.
  2. Tarehe 29 Desemba, 2023, TMDA ilipokea taarifa iliyotolewa na taasisi ya Udhibiti Chakula na Dawa nchini Rwanda (Rwanda FDA) juu ya uwepo katika soko la nchi hiyo wa matoleo duni ya dawa aina ya Fluconazole ya vidonge ya miligramu 200 yaliyotengenezwa na kiwanda cha Universal Corporation kilichopo Kikuyu nchini Kenya katika Kitalu Na.13777, Club Road. Matoleo duni ya dawa hiyo ni Na. 5810315, 5810316, 5811390 na 5810022 na kuisha muda wake wa matumizi, Agosti, 2025.
  3. RFDA imefanya hivyo ili kutekeleza matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kutoa taarifa za uwepo wa dawa duni na bandia ili Mamlaka zingine za Udhibiti wa Dawa duniani nazo ziweze kuchukua hatua iwapo matoleo husika yatakuwa yamesambazwa katika nchi zao.
  4. TMDA inapenda kuujulisha umma kuwa haijasajili dawa hiyo ya vidonge (Fluconazole 200 mg tablets) badala yake imesajili dawa hiyo ikiwa katika mfumo wa kapsuli za miligramu 150 na 200 (Fluconazole 150mg and 200mg Capsule) kutoka kiwanda hicho.
  5. Aidha, tunapenda kuujulisha umma kuwa TMDA haijatoa kibali cha kuingiza dawa hiyo nchini. Hata hivyo, kwa kuwa kuna uwezekano wa dawa hiyo kuingizwa nchini kwa njia haramu na mipaka isiyo rasmi, TMDA ilichukua hatua ya kufuatilia katika soko la nchi yetu na kujiridhisha kuwa matoleo tajwa ya dawa hiyo hayajaingizwa nchini.
  6. Mamlaka itaendelea kufanya ufuatiliaji zaidi wa dawa zilizosajiliwa kutoka kiwanda hicho pamoja na viwanda vingine kwa lengo la kuendelea kulinda afya ya jamii.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Jengo la PSSSF, Ghorofa ya 10, Barabara ya Makole,
S. L. P 1253, Dodoma au
S. L. P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Nukushi: +255 22 2450793
Simu bila malipo: 0800110084