Latest News
Posted On: Oct 09, 2019

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA

TAARIFA KWA UMMA

Oktoba 04, 2019

MATANGAZO YA DAWA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII

  1. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ni Wakala wa Serikali chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
  2. TMDA inapenda kuutangazia umma kuwa kumekuwepo na utangazaji au uwekaji wa taarifa za dawa kwenye mitandao ya kijamii bila ya kuwa na kibali maalum kutoka Mamlaka. Mitandao hiyo ni kama Whatsapp, Blogs, Facebook, Twitter, Youtube, Instagram, LinkedIn, MySpace, Pinterest na kadahalika.
  3. Matangazo hayo ni kinyume na Kanuni za Udhibiti wa Matangazo ya Dawa na Dawa za Mitishamba za 2010 (Tanzania Food, Drugs and Cosmetics (Control of Drugs and Herbal Drugs Promotions) Regulations, 2010).
  4. Aidha, dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari (Prescription Only Medicines) haziruhusiwi kutangazwa kwenye vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii. Matangazo ya dawa ni lazima yapewe kibali cha kutangazwa kutoka TMDA.
  5. Kwa taarifa hii, TMDA inawaelekeza waingizaji, wauzaji, wasambazaji wote wa dawa na umma kwa ujumla, kuacha kuweka matangazo yoyote ya dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari kwenye mitandao hiyo na kuhakikisha kuwa matangazo ya dawa yanayotolewa yanakuwa na taarifa za matumizi sahihi ya dawa na yameidhinishwa na Mamlaka kutumika kutangaza dawa husika.
  6. TMDA inatoa rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa ikiwa watabaini kampuni, kikundi, mitandao au mtu yeyote anayejihusisha na utangazaji wa dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari kwenye mitandao ya kijamii hapa nchini.
  7. Aidha, hatua stahiki zitachukuliwa kwa wale watakaoendelea kutangaza dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari kwenye mitandao ya kijamii hapa nchini.
  8. TMDA itaendelea kufanya udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa Dawa na Jukumu la kulinda afya ya wananchi ni letu sote hivyo wadau wote tushirikiane katika kutekeleza maagizo haya kwa mujibu wa kanuni.
Imetolewa na:
Kaimu Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),
Mtaa wa Mwanza, Kitalu T, Kiwanja Na.6
S.L.P 1253, Dodoma Au
S.L.P 77150, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2452108/2450512/2450751
Simu bila Malipo: 0800110084