Latest News
Posted On: Nov 13, 2019

MAMLAKA YA DAWA NA VIFAA TIBA

TAARIFA KWA UMMA

MATOKEO YA UKAGUZI MAALUM (OPERESHENI) WA DAWA VIFAA TIBA, VITENDANISHI, DAWA ASILI NA TIBA MBADALA

Imetolewa na Akida M. Khea
Kaimu Mkurugenzi Mkuu

13 November, 2019

Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu, Maabara za Wakala wa Veterinari

Mwakilishi wa Msajili, Baraza la Famasi,

Msajili, Baraza la Dawa Asili na Tiba Mbadala,

Mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais,

Mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi,

Wakurugenzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba,

Wanahabari,

Mabibi na Mabwana,

Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kuwakaribisha Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na kuwashukuru wote kwa kuitikia wito wa kuja kupokea taarifa kwa umma kuhusu matokeo ya ukaguzi maalum (operesheni) ya ukaguzi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi, dawa asili na tiba mbadala uliofanyika kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba, 2019 katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, maghala na maduka ya dawa za binadamu na mifugo.

Ndugu wanahabari,

Naomba kuwataarifu kuwa TMDA kwa kushirikiana na Ofisi ya Raisi, Baraza la Famasi, Baraza la Dawa Asili na Tiba Mbadala na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia watalaam wa dawa waliopo katika Halmashauri ilifanya ukaguzi maalum (operesheni) katika wilaya 33 za mikoa 20 iliyopo katika ofisi zote za Kanda za TMDA yaani Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Tanga, Ruvuma na Mtwara), Kanda ya Kaskazini (Arusha na Kilimanjaro), Kanda ya Kati (Dodoma, Morogoro na Singida), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Iringa, Songwe na Rukwa), Kanda ya Magharibi (Kigoma na Tabora) na Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, Shinyanga, Geita na Kagera).

Lengo la ukaguzi maalum huu lilikuwa ni kubaini, kukamata na kuondoa katika soko dawa duni na bandia za binadamu na mifugo, vifaa tiba na vitendanishi ambavyo havijasajiliwa au havijatambuliwa (notified) na TMDA, na pia dawa asili na tiba mbadala ambazo hazijaruhusiwa kutumika nchini. Vilevile, ukaguzi huu ulifanyika kufuatia taarifa ya kuwepo kwa matukio kadhaa ya dawa duni na bandia katika baadhi ya nchi zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kipindi cha Julai – Septemba, 2019.

Ndugu wanahabari,

Mtakubaliana nami kuwa tatizo la dawa na vifaa tiba bandia lipo katika nchi zote duniani ikiwa ni pamoja na nchi zilizoendelea. Hii inamaanisha kuwa tatizo hili ni la uhalifu unaovuka mipaka ya nchi moja kwenda nchi nyingine (cross border crime).

Hivyo, dawa na vifaa tiba bandia zinapobainika, kutolewa taarifa na kuthibitishwa katika nchi moja popote duniani taarifa zake husambazwa kupitia mifumo ya kiudhibiti (regulatory and enforcement systems) na kutumwa Shirika la Afya Duniani (WHO) ili nchi nyingine zichukue tahadhari kwa kufanya ukaguzi wa kuzuia, kubaini na kukamata / kuondoa dawa na vifaa tiba bandia katika soko na kuutarifu umma ili pia uchukue tahadhari kwa lengo la kulinda afya ya jamii.

Katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019, baadhi ya dawa bandia zilizobainika na kutolewa taarifa ya kuwepo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ambazo tayari TMDA imeshatoa taarifa kwa umma (press release) kupitia tovuti yake ni pamoja na dawa aina ya Gentrisone Cream 10gm toleo namba GNTRO X030, Augmentin 625mg tablets toleo namba 786627 na kapsuli za Cold caps. Viwanda halisi vinavyotengeneza dawa hizi vilithibitisha kuwa dawa hizo hazikutengenezwa na viwanda husika. Aidha, kwa mujibu wa uchambuzi na uchunguzi uliofanywa na TMDA, matoleo tajwa ya dawa husika yalithibitishwa kuwa ni bandia.

Kwa mfano, uchunguzi kupitia maabara ya TMDA kwa dawa ya Gentrisone cream 10gm toleo namba GNTRO X030 ulionesha kuwa dawa hiyo haikuwa na viambato hai (active pharmaceutical ingredients) vya dawa hiyo ambavyo ni Betamethasone Proprionate, Clotrimazole na Gentamycin sulfate.

Ndugu wanahabari,

Kwa kuzingatia taarifa za mifumo ya ukaguzi na udhibiti za TMDA na taarifa nyingine kutoka vyombo vya usalama nchini, operesheni hii ilielekeza nguvu zake katika mikoa inayopakana na nchi jirani hususan mikoa ya Kigoma, Songwe, Kagera, Rukwa, Mbeya, Mara, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza, Ruvuma, Mtwara na Tanga. Aidha, mikoa mingine iliyokaguliwa ni pamoja na Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Geita, Singida, Morogoro, Iringa na Tabora. Hivyo, katika operesheni hii jumla ya maeneo 558 ikiwa ni famasi 209, Maduka ya Dawa Muhimu 263, Vituo vya kutolea huduma za afya 27, Maduka ya Vifaa Tiba 21 na Vituo vya dawa asili na tiba mbadala 38 yalikaguliwa kama ifuatavyo;-

Jedwali Na.1: Idadi ya maeneo yaliyokaguliwa

Na. Mkoa Famasi Maduka ya Dawa Muhimu Vituo vya Huduma za Afya Maduka ya Vifaa Tiba Vituo vya Tiba Asili na Tiba Mbadala Jumla
1.Dar es Salaam60 3310 076
2.Tanga6 200 08
3.Mtwara 2 620 010
4.Ruvuma6 2340 134
5.Arusha30 684 856
6.Kilimanjaro 16 1832 241
7.Shinyanga12 800 626
8.Mara2 3040 238
9.Geita9 3700 046
10.Mwanza9 400 013
11.Dodoma16 531 227
12.Singida6 1300 423
13.Morogoro17 700 529
14.Iringa8 2300 233
15.Mbeya3 1202 221
16.Kigoma5 3100 040
17.Rukwa0 1000 010
18.Songwe0 200 02
19.Tabora2 900 011
20.Kagera0 1400 014
Jumla209 2632721 38558

Ndugu Wanahabari,

Katika ukaguzi huu maalum, aina saba (7) ya dawa bandia zenye thamani ya TZS 12,495,500/= zilikamatwa. Majina ya dawa hizo na sampuli zake ni kama ifuatavyo:-

Jedwali namba 2: Aina ya dawa bandia zilizokamatwa

Na. Jina la dawa Idadi Maelezo
1. Sonaderm Cream 10gm (Clobetasol Proprionate, Miconazole, Nitrate & Gentamicin Sulphate ) Tube 1,010

Sonaderm cream toleo namba A1912 na A1758 ni bandia.

Uchunguzi katika maabara ya TMDA na taarifa kutoka kiwanda cha Blue Cross Laboratories Ltd, India kinachotengeneza dawa halisi umethibisha kuwa matoleo tajwa ya dawa hii hayana viambato hai hivyo ni bandia.

2. Gentrisone Cream 10gm (Betamethasone Proprionate, Clotrimazole & Gentamycin sulfate) Tube 17

Gentrisone cream toleo namba GNTRO X030 na tarehe ya kutengenezwa 21/04/2019 ni bandia.

Uchunguzi katika maabara ya TMDA na taarifa kutoka kiwanda cha Shin Poong Pharm. Co. Ltd, Korea ya Kusini umethibitisha kuwa toleo tajwa la dawa hiyo halina viambato hai hivyo ni bandia.

3. Sulphadoxine Pyrimethamine Kopo lenye vidonge 800 Kopo la dawa husika lina namba ya kughushi ya usajili namba TAN 05.412.102.FAST
4. ALPRIM (Sulfamethoxazole 400mg +, Trimethoprim 80mg) tablets Makopo 39@ vidonge 1000

ALPRIM toleo namba 6L74 na tarehe ya kutengenezwa Oktoba, 2018 ni bandia.

Taarifa kutoka kiwanda Elys Pharmaceutical Industries, Kenya zimethibitisha kuwa dawa hizo ni bandia.

5. Homidium Chloride Makopo 9 @vidonge 100 Makopo matatu (3) ya dawa hii ya mifugo yanaonesha yametengenezwa na kiwanda cha Cipla, India ambacho hakitengenezi dawa za mifugo na makopo mengine sita (6) yanaonesha yametengenezwa na kiwanda cha Malleus Chem Ltd, Nairobi Kenya na kuonesha kutambuliwa na PPB, Kenya taarifa ambayo siyo ya kweli na kuthibitisha kuwa dawa hiyo ni bandia
6. Cold cap Kapsuli 396 Dawa hii inadaiwa kutengenezwa nchini India ambapo jina la kiwanda halipo katika kifungashio wakati dawa halisi COLDCAP inatengenezwa na kiwanda cha Regal Pharmaceuticals Ltd, Nairobi, Kenya. Hivyo ni bandia.
7. TEMEVAC NDV strain I&2 (chanjo ya kuku kwa ajili ya ugonjwa wa mdondo). 125 vials

Dawa hii bandia imeandikwa kwa kiingereza na ina makosa ya kisarufi katika lebo na inaonesha imetengenezwa na kiwanda cha Vaccine Institution of Holland.

Taarifa kutoka kwa kiwanda cha Serikali kinachotengeneza dawa halisi cha TVI Kibaha, Tanzania imethibitisha kuwa dawa hiyo ni bandia na haina viambato hai vyovyote

Hata hivyo, naomba nifafanue na kueleweka kwa umma kuwa pamoja na kubainika kwa uwepo wa dawa hizi bandia, zipo dawa halisi na zilizosajiliwa na TMDA zenye majina haya. Hivyo, kilichofanywa na wahalifu ni kutumia majina ya dawa hizi kughushi dawa hizo ili kuwadanganya wananchi kuwa dawa hizo ni halisi.

Ndugu wanahabari,

Ukaguzi huu maalum, pia ulikamata dawa ambazo hazijasajiliwa zenye thamani ya TZS 31,934,360/= baadhi yake zikiwa kapsuli za dawa inayotambulika kwa jina la Indowin, vidonge vya dawa yenye mchanganyiko wa Artesunate na Amodiaquine, kapsuli za dawa inayojulikana kwa jina la Coldwin na dawa ya sindano ya Magnesium Sulphate.

Pia katika ukaguzi huu maalum, dawa za serikali zenye thamani ya TZS 481,600/= baadhi yake zikiwa ni vichupa vya dawa ya Sindano ya Oxytocin , Vidonge vya dawa inayoitwa Bigomet, Vichupa tisa (9) vya dawa ya sindano inayoitwa Depo provera, dawa za vidonge vya kutibu malaria Lumartem (Artemether 20mg +Lumefantrine 120mg) kozi 32 na Vidonge vya dawa yenye mchanganyiko wa Ferrous Sulphate na Folic Acid zilikamatwa katika maduka ya dawa ya watu binafsi

Aidha, vifaa tiba duni vyenye thamani ya TZS 640,000/= kati yake vikiwa ni surgical blades na H.pylori rapid test na pia vifaa tiba vya Serikali vyenye thamani ya TZS 224,300/= baadhi yake ni vifaa vya SD Bioline kwa ajili ya kupima HIV, kaswende na malaria vifaa tiba aina ya cannula na pamba (cotton wool) vilikamatwa.

Operesheni pia ilibaini na kukamata vifaa tiba ambavyo havijasajiliwa vyenye thamani ya TZS 16,384,750/= ambavyo baadhi yake ni Magnetic Quantum analyser (3), Quantum therapy analyzer (1) na aina mbalimbali ya kondomu kama vile ultimate condoms, classic maximum protection na prudence condoms.

Ndugu wanahabari,

Kutokana na matokeo ya Operesheni hiyo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ambapo hatua ya kwanza ilikuwa ni kuziondoa dawa duni na bandia, vifaa tiba na vitendanishi ambavyo havijsajiliwa / kutambuliwa na TMDA katika maeneo yote zilipopatikana ili kulinda afya ya jamii.

Aidha, kwa maeneo yote yaliyopatikana na dawa bandia, dawa au vifaa tiba au vitendanishi vya Serikali watuhumiwa walifikishwa katika vyombo vya usalama ambapo jumla ya majalada 19 ya kesi yalifunguliwa katika vituo mbalimbali vya Polisi nchini ambapo mara baada ya uchunguzi wa makosa kukamilika kupitia Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali hatua mbalimbali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani kulingana na Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219 na Sheria nyingine za nchi.

Aidha, ufuatiliaji kupitia vyombo vya usalama unaendelea kuwabaini wale wote wanaojihusisha na uingizaji, utengenezaji na usambazaji wa dawa bandia kwa lengo kujipatia kipato kinyume cha Sheria na kuathiri afya za wananchi.

Ndugu wanahabari,

Kufuatia matokeo ya ukaguzi maalum, naomba kutoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapata dawa kutoka katika vituo vya kutolea huduma za dawa vinavyotambuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na maduka ya dawa yaliyosajiliwa na Serikali kupitia taasisi zake na kuhakikisha wanapewa risiti zilizoandikwa dawa walizopewa.

Aidha, natoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara waliouziwa dawa hizi bila kujua kutoa taarifa TMDA au katika vyombo vya usalama ili hatua za kuwabaini wanaosambaza dawa hizo zichukuliwe. Endapo kuna wananchi watabaini kuwa na matoleo ya dawa zilizobainishwa kuwa ni bandia, wanashauriwa wazirudishe dawa hizo katika ofisi za TMDA au ofisi za Serikali zilipo karibu nao ili kuhakikisha dawa hizo zinatoka katika mzunguko wa matumizi.

Aidha, kwa lengo la kulinda afya ya jamii, wananchi wanaombwa kutoa taarifa kuhusu watu, makundi au mtandao wa wale wote wanaojihusisha na uingizaji nchini au utengenezaji hapa nchini wa dawa bandia, wizi wa dawa za serikali, vifaa tiba na vitendanishi ambavyo hazijasajiliwa au kutambuliwa kwa kuwa bidhaa hizi ni hatari kwa afya ya jamii.

Ndugu wanahabari,

Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa taasisi zilizoshirikiana na TMDA katika kufanikisha operesheni hii ambazo ni Baraza la Famasi, Baraza la Dawa Asili na Tiba Mbadala, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kutambua umuhimu wa zoezi hili na kushiriki kwa maslahi ya Taifa. Aidha, TMDA inatambua mchango wa ushauri ambao umetolewa na wadau wengine ikiwa ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Jeshi la Polisi Tanzania, Wakala wa Maabara za Veterinari, Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Bohari ya Dawa, na Baraza la Veterinari na wananchi kwa ujumla.

TMDA kwa upande wake itaendelea kuhakikisha kuwa inatumia mifumo yake thabiti ya ukaguzi na udhibiti katika kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyoingizwa na kusambazwa nchini ni bora, salama na vyenye ufanisi.

Mwisho napenda kipekee niwashukuru wanahabari kwa kuhudhuria mkutano huu.

Aksanteni kwa kunisikiliza